Wapentekoste

"Apostolic Faith Mission" kwenye Azusa Street inahesabiwa kuwa chanzo cha tapo la Kipentekoste.
Waumini wa Pentecostal Church of God huko Lejunior, Kentucky, Marekani wakimuombea msichana mwaka 1946.


Wapentekoste ni jina linalojumuisha Wakristo wanaofuata tapo la Kipentekoste linalolenga kuleta upyaisho katika Kanisa kwa kutia maanani tukio la sikukuu ya Pentekoste ya mwaka uleule wa kifo na ufufuko wa Yesu.[1]

Tapo hilo linaungana na Waprotestanti wengine katika kushikilia Biblia ya Kikristo tu na kwa njia yake kumkiri Yesu kuwa Bwana na kumpokea kama mwokozi, lakini pia linasisitiza mang'amuzi binafsi ya Roho Mtakatifu katika maisha ya muumini kama yalivyotokea mwanzoni kadiri ya Matendo ya Mitume ili kuwezeshwa kuishi Kikristo kweli kwa upako wa Roho.

Kwa kuwa wanajitangaza "wameokoka", yaani wameachana na dhambi, kwa Kiswahili wanaitwa pia "Walokole".

Tangu tapo hilo lilipoanza mwaka 1907 huko Marekani, Wapentekoste wameshakuwa zaidi ya milioni 279, mbali ya Wakristo wa madhehebu ya zamani walioathiriwa nalo ambao wanaitwa mara nyingi Wakarismatiki na ambao idadi yao inalingana na hiyo.

  1. "Spirit and Power: A 10-Country Survey of Pentecostals", Executive Summary Ilihifadhiwa 30 Julai 2013 kwenye Wayback Machine.. The Pew Forum on Religion and Public Life.

From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne