Wilaya ya Tunduru ni wilaya mojawapo kati ya 8 za Mkoa wa Ruvuma, nchini Tanzania. Kwa upande wa kusini Tunduru inapakana na nchi ya Msumbiji, upande wa magharibi na wilaya ya Namtumbo, kaskazini na mkoa wa Lindi na upande wa mashariki imepakana na Mkoa wa Mtwara.[1]
Wilaya ya Tunduru ni moja ya wilaya kongwe nchini kwa kuwa ilianzishwa mwaka 1905 wakati wa ukoloni. Serikali ya Ujerumani ilijenga boma katika eneo la Kadewele karibu na lilipo jengo la Mamlaka ya Mapato TRA kwa sasa.
Katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002, idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ilihesabiwa kuwa ni watu 247,976 [2]. Katika sensa ya mwaka 2022 walihesabiwa 412,054 [3]. Walio wengi ni kabila la Wayao.
Wilaya ina tarafa 7 ambazo ni Mlingoti, Nalasi, Nakapanya, Nampungu, Matemanga, Lukumbule, Namasakata na Mbesa kwa Tunduru mjini.
Wilaya ya Tunduru kuna shule za sekondari na shule za msingi ambazo baadhi ya shule hizo ni Tunduru Sekondari, Mataka, Frank Weston na Masonya.
Pia wilaya hiyo ina Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Nandembo (Nandembo FDC), ambacho kipo katika kijiji cha Nandembo, na Chuo cha Biblia cha Kanisa la Biblia Tanzania huko Nanjoka.