Mathayo anathibitisha hilo kwa kutaja utabiri wa maneno ya Isa 7:14 katika tafsiri ya Kigiriki ya Septuaginta: "Tazama bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana, nao watamwita jina lake Emmanuel, yaani Mungu pamoja nasi".[3][4]
↑1:18Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. 19 Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri. 20 Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, "Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. 21 Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye atawaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao." 22 Basi, haya yote yalitukia ili litimie lile neno Bwana alilosema kwa njia ya nabii: 23 "Bikira atachukua mimba, atamzaa mtoto wa kiume, naye ataitwa Emanueli" (maana yake, "Mungu yu pamoja nasi"). 24 Hivyo, Yosefu alipoamka usingizini alifanya kama malaika huyo alivyomwambia, akamchukua mke wake nyumbani. 25 Lakini hakumjua kamwe kimwili hata Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu.
↑1:26 Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, 27 kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. 28 Malaika akamwendea, akamwambia, "Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe." 29 Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini? 30 Malaika akamwambia, "Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. 31 Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu. 32 Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. 33 Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho."
34 Maria akamjibu, "Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?" 35 Malaika akamjibu, "Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. 36 Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa. 37 Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu." 38 Maria akasema, "Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema." Kisha yule malaika akaenda zake.