| |
Mahali | Afrika ya Mashariki |
Nchi zinazopakana | Tanzania, Uganda na Kenya |
Eneo la maji | 68,100 km² |
Kina cha chini | 81 m |
Mito inayoingia | Kagera, mto Katonga, mto Nzoia n.k. |
Mito inayotoka | Nile |
Kimo cha uso wa maji juu ya UB |
1,134 m |
Miji mikubwa ufukoni | Kampala, Kisumu, Mwanza |
Ziwa Viktoria (pia: Ziwa Nyanza au Ziwa Ukerewe) ni ziwa kubwa la Afrika ya Mashariki lililopo baina ya Tanzania, Kenya na Uganda. Eneo la maji ya ziwa limegawanywa 49% (km2 33,700) nchini Tanzania, 45% (km2 31,000) nchini Uganda, na 6% (km2 4,100) nchini Kenya.
Ziwa Viktoria lipo mita 1134 juu ya usawa wa bahari na lina eneo la kilometa za mraba zaidi ya 68,100. Hivyo ni ziwa kubwa kuliko yote barani Afrika, na la pili duniani, baada ya Ziwa Superior ambalo lipo Amerika ya Kaskazini.
Ziwa hili linapata maji yake mengi kutokana na mvua (80%) na kutoka vijito vingi vidogo. Mto mkubwa unaoingia Viktoria ni Mto Kagera unaotiririka kutoka magharibi.
Maji ya ziwa Viktoria yanatoka na kumiminika kwenye mto Nile na kuelekea bahari ya Mediteranea kwa umbali wa maili 4,000.
Ziwa hilo lina kina cha wastani cha mita 40 na mwambao wa urefu wa kilomita 4,828, visiwa vyake vikiwa vimechangia 3.7% ya urefu huu.
Ziwa hilo liliwahi kukauka kabisa mara kadhaa tangu lilipoanza miaka 400,000 iliyopita.